SEHEMU YA TANO
Mada Ndogo: Njia 8 za kuyashinda mapepo.
Bwana Yesu asifiwe sana,
Ndugu mpendwa, katika sehemu Nne zilizotangulia,tumejifunza
maana,asili/ chanzo cha mapepo na dalili kuu za mtu alievamiwa na
mapepo. Natumai umebarikiwa sana. Haleluya! Ndugu mpendwa, napenda
kukukaribisha katika mwendelezo wa mafundisho yetu juu ya mapepo,ambapo
kwasasa tutaangalia kwa kina mbinu/njia za kumshinda pepo.
Ndugu yangu mpendwa, kanisa la leo, liko katika mapambano makubwa sana.
Upinzani mkubwa unatoka kwa ibilisi alie shetani, mwenye sifa kuu ya
uharibifu.
Hatahivyo, Mungu ameliweka kanisa kwa wakati huu wa
mashambulizi kwaajili ya kuukomboa ulimwengu. Amelifanya kanisa kama
asikari wa mwamvuli ambaye hushushwa katikati ya eneo ambalo bado liko
mikononi mwa adui, ila ikikusudiwa kupambana na hata kushinda. Kwa
mantiki hiyo, si hoja tena juu ya kushinda kwa kanisa, bali daima
linashinda na litaendelea kushinda.
Katika mwendelezo wa somo letu, leo tutaziangalia njia/uwezo wa kuyashinda mapepo.
Kwanza; Yesu alitoa mamlaka kwa kanisa juu ya mapepo (Marko 16:17).
Uweza huu wa ajabu, Mungu ameutoa kwa watu wote wanaomwamini Yesu Kristo
kuwa Bwana na Mwokozi wao (Yohana 17:20-23). Ujue, watu wengine
wanateseka kwa kuwa hawajui, yule aliye ndani yao. Biblia inasema,
aliyeko ndani ya aliyeokoka ni mkubwa mno, maana yake ni kuwa,
anayashinda mapepo. Usikubali kuteswa na mapepo, kemea kwa jina la Yesu,
lililo jina kuu kupita majina Yote, nawe utakuwa huru.
Pili; Mapepo
huamriwa kwa jina la Yesu tu (Marko 16:17). Jina maagano na ahadi ni
jina la Yesu tu. Usitumie jina lingine lolote lililo nje ya jina la
Yesu. Ni jina la Yesu pekee huweza kuponya,kuokoa na kuhuisha, hata
mapepo yanajua hivyo. Kutumia majina mengine ni sawa na kukosea anwani
wakati wa kutuma barua, ni kweli barua itaenda ila usitegemee kupokea
majibu uliyotarajia kwa kuwa barua haitaenda kwa mlengwa.
Tatu;
Yafukuize kwa kutumia mamlaka uliyonayo kama ilivyoelezwa katika hoja ya
kwanza. Usiyabembeleze. Tumia amri. Watu wengine hutumia majadiliano,
huyafanyia sherehe, huyafukizia uvumba,udi na hata kuyachezea muziki wa
asili. Ndugu yangu, waswahili wanasema” ukifanya urafiki na mkia wa
fisi,utakufirisi” usikubali kukaa meza moja na mapepo, shetani
habembelezwi, yatimue kwa mamlaka ya Jina la Yesu (Mathayo 12:28,Luka
11:20).
Nne; Usiyaruhusu kujieleza. Mpiganaji mzuri, hamuulizi adui
ametoka wapi, yeye hushambulia hata kikosi kizimahukimaliza, kwa kuwa ni
jasili na anajiamani, hababaishwi. Usikubalia kuhojiana na pepo, pepo
ni waongo, watakudanganya kwa kutoa habari za uongo ili kulibomoa kanisa
(mwili wa kristo) ili kuwatenganisha. Wataibua uadui kati yenu. We
yaaamuru yaondoke, hata Yesu mwenyewe aliyaamuru tu yakaondoka (Luka
4:41,Marko 1:34).
Tano; Kwa kufunga na kuomba (Marko 9:29). Ndugu
yangu mpendwa, kila mara, adui hushinwa kwa sala na kusoma neno. Jaama
mamlaka ya mbinguni ili kumshinda ibilisi. Mtu asiye na maombi ni sawa
na bunduki isiyo na risasi, na mtu asiyeomba anafanana na mlinzi
anaetegea kazi yake, hutoa mwanya kwa mwizi kuvamia na kupora. Usikubali
kuwa mlango wa ulegevu, daima jitahidi kuwekeza neno kwa wingi ili
ujipatie maarifa zaidi.
Sita; Kuwa na Imani thabiti (Mathayo
17:19-20). Maombi pasipo imani, ni sawa na dhihaka. Ni bora ya
majaribio, kuliko kudhihaki. Daima, kuwa jasili na umwamini Mungu na
neno lake, ndipo litatimia kwako. Mtu asiyeamini, maombi yake
hupeperushwa na mawimbi,hivyo hata majibu ya maombi yake hupeperushwa
tu,kwakuwa hayana nguvu yoyote ndani yake.
Saba; Kwa Kumwamini Mungu
(Marko 6:5&6), ukimwamini utamtegemea kwa kila jambo(Marko
9:23&24). Ukiwa na imani kwake, utakuwa na ujasili. Mwamini
Mungu,ili athibitishe ujasili wako.
Nane; Kwa Muujiza. Mungu, ni
Mungu wa maajabu, hufanya mambo yaliyojuu ya fahamu za mwanadamu.
Hufanya mambo ya kushangaza, kuweza kufanya miujiza mikubwa mno,amabayo
hata uwezo wa wasomi,hufikia kikomo. (Matendo 19:11&12), tunaonao
nguo za Paulo zikifanya maajabu, ni muujiza wa nguo kutoa pepo. Ni kwa
kuwa kuna upako unaokuwa sambamba na wamchao Bwana. Tegemea Miujiza kama
uko kwenye uwepo muda wote. Kumbuka, imani wakati mwingine haionekani
(Matendo 16:16-19), hivyo miujiza huithibitisha imani.
Swali la kujiuliza ni je, kila mtu anaweza kumtoa pepo?
Jibu ni Hapana, si kila atakaye tumia jina la Yesu anaweza kutoa pepo,
tena anaweza hata kujikuta yuko kwenye wakati mgumu zaidi kwa kuwa jina
la Yesu lina uwezo wa ajabu, hivyo mtu anapaswa kulitumia kama silaha
huku akihakikisha amejilinda vizuri mahali alipo (Matendo 16:13-16), mtu
asiyejulikana katika ufalme wa Mungu, anapoliita jina la Yesu, huwa
kama mtoto anaemlilia mama asiye wake, hata akimuonea huruma vipi,
hawezi kuwa mama yake kabisa. Hii ni kwasababu, hawana utambulisho kwa
Yesu, japo wanatumia jina lake(Luka 7:22&23).
Ifahamike kuwa,
mtu ambaye hajamwamini Yesu,pengine ni mpagani kabisa, akiombewa, pepo
hutii amri ya mwombaji na kuondoka, lakini kwa kuwa anayeombewa
hajaamini, yule pepo huweza kurudi na kufanya makao tena ndani yake. Ni
sawa na mpiganaji vitani anaevamia, na kupamabana na kuondoka bila
kuacha walinzi. Adui, anakuwa na uwezo wa kurudi tena na kujimilikisha
na hata akaweka ulinzi wake ulio imara zaidi kuliko ule wa awali
(Mathayo 12:44&45).
Ndugu mpendwa, naimani unaendelea kubarikiwa
kwa mafundisho yetu. Huu ndiyo utakuwa mwisho wa mada yetu. Usikose
mada zijazo. Mungu akubariki.
Mwl. Sospeter Simon S. Ndabagoye
New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania
No comments:
Post a Comment