Sehemu ya Pili
Jambo la Pili
Unapoamua kuoa au kuolewa, fahamu ya kwamba hiyo ndoa
inakuunganisha na kukuingizakatika familia nyingine.
Unapoamua kuoa au kuolewa, fahamu ya kwamba hiyo ndoa
inakuunganisha na kukuingizakatika familia nyingine.
Unafahamu watu wengi sana wakioa au kuolewa wanafikiria tu
mahusiano ya wao wenyewe tu; na hii ni hatari sana. Kwa sababu unapooa unaingia
kwenye undugu na familia nyingine kabisa tofauti, na sio mahusiano ya kwenu tu
wawili. Ninyi ni kigezo tu cha kuunganisha hizo familia mbili, lakini
mkiishaoana hizo familia zenu mbili ni ndugu kuanzia wakati huo.
Ndio maana unapofika unataka kuoa au kuolewa, sio suala la
kumtazama kijana tu, au kumtazama msichana yeye mwenyewe tu; kwa mfano
alivyosoma, lakini ni lazima pia utazame na hali ya familia yake ili ujue
unajiingiza kwenye familia ya namna gani. Unapofika kwenye masuala ya namna
hiyo kuna vitu vingi sana vya kuangalia.
Unaweza ukaingia kwenye familia ambayo ni wavivu, mimi
ninakuambia jasho litakutoka ukioa msichana wa namna hiyo; au ukipata kijana
toka kwenye familia ya namna hiyo. Itakuwa kazi sana kumshawishi mwenzako juu
ya kujishughulisha na maisha. Maana inategemea; kwa kuwa unaweza kuoa msichana
hata kusonga ugali hajui. Sisi kwenye nyumba ya baba yetu, hatuna msichana,
tumezaliwa watoto wa kiume watupu, msichana wa kwanza kuingia kwenye familia
yetu ni mke wangu.
Lakini mama yetu alikuwa na bidii ya kutufundisha kila kitu,
alitufundisha kupika, alitufundisha kufuma, alitufundisha kusuka nywele. Kwa hiyo
nilijifunza kwanza kusuka tatu kichwa. Lakini sikuanzia kujifunzia kusuka
nywele kwenye kichwa cha mtu, bali nilijifunzia kwenye majani; wao wakikaa
wanasuka hapo na sisi tuko hapo tunafundishwa jinsi ya kusuka kwenye majani.
Sasa wengine hawapati nafasi ya namna hiyo, na ni mbaya zaidi kwa
wasichana. Mungu amenipa nafasi ya kuwa na watoto wakike watatu na wa kiume
mmoja, itakuwa ni aibu kwetu kama wazazi, ikafika wakati wanaingia katika ndoa
zao na hawajui kupika ni aibu; kwa hiyo lazima wajue kupika. Maana kwa
kujua hilo anaonyesha anatoka familia ya namna gani, na imemlea kwa namna gani!
Unaweza ukafikiri unamlea mtoto wako vizuri, maana siku hizi kuna
shida ya kuwa na wafanya kazi majumbani mwetu. Ukishakuwa na mfanyakazi
nyumbani basi watoto wengine hawafanyi kitu, wakati mwingine wanakula
chakula na wanaacha sahani hapo hapo mezani.
Kuna watoto wengine inakuwa mpaka yuko sekondari hawezi kufua nguo
zake. Kwa kuwa nyumbani kama hakuna wa kumfulia basi kuna mashine za kufulia.
Huko unakokwenda kuolewa inawezekana hata mashine ya kufulia hawajawahi kuiona!
Unafika pale na unauliza mashine iko wapi, wanakuambia yakufanyia nini, - ya
kusagia mahindi? Maana ndio wanayoijua kuwa ndio mashine!
Hujui hata namna ya kushika kioo cha taa ya chemli wala
namna ya kuiosha kule ndani lile vumbi likaondoka. Inawezekana mwingine
umezaliwa kwenye nyumba yenye umeme, lakini utakapokuwa katika ndoa unaenda
kwenye nyumba ambayo haina hata umeme, unafika kule na unashangaa kweli maana
hujui hata namna kuwasha taa ya chemli! Kwa hiyo tunawaambia watoto wetu suala
la kujifunza hivi vitu sio suala la kuchagua, hata kama kuna mtu pale nyumbani
wa kuwasaidia, ni lazima wajue kufanya kazi!
Nilienda kwenye mkoa mmoja wakasema, sisi ukitaka kuoa kwenye
nyumba ya mtu, ukitaka kujua huyo msichana amelelewa vizuri au vibaya wakasema
usimtazame alivyovaa. Badala yake wanafika kwenye uwanja wa nyumba ya wazazi
wake, na wanaangalia ile barabara inayokwenda nyumbani kwao, na wakiikuta
chafu, basi wanajua huyu msichana ni mchafu, hawahangaiki tena kuja kuzungumza,
wanajua hapa kama tunaamua kuoa tujue tunacho oa, huyu msichana ni mchafu!
Ukienda kuoa kwenye familia nyingine utakuta wanasumbuliwa na
ugonjwa wa kurithi, na usipojua kitu cha kufanya unaweza ukapata shida sana.
Lakini ninachotaka kukuambia ni kwamba, uamuzi wa kuoa au kuolewa unakuingiza
kwenye familia nyingine kabisa, na inaunganisha hiyo familia yao na
familia yako; kwa hiyo hayo sio maamuzi madogo. Kumbuka unapooa au
kuolewa unawaingiza watu katika famila ambazo kama usipokuwa mwangalifu
inaweza ikaleta shida sana, lakini pia inaweza ikaleta baraka!.
No comments:
Post a Comment