Wiki ya Nne
Jambo la Nne
Uamuzi wa kuoa au kuolewa ni muhimu uwe mwangalifu nao,
kwa sababu utakufanya uwajibike zaidi.
Uamuzi wa kuoa au kuolewa ni muhimu uwe mwangalifu nao,
kwa sababu utakufanya uwajibike zaidi.
Kama hujawa mtu wa kuwajibika, basi, hujawa tayari kuwajibika, kwa
hiyo usiingie kwenye ndoa! Kuoa au kuolewa kunakufanya uwajibike zaidi, maana
yake ni kutafuta wajibu mkubwa zaidi.
1Timotheo 5:8 anasema, “Lakini mtu ye yote asiyewatunza
walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya
kuliko mtu asiye amini”, maana yake ni mbaya kuliko mtu ambaye hajaokoka.
Afadhali mtu yule ambaye hajaokoka. Huyo ambaye ameokoka, lakini hatunzi watu
wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, maana yake amemkana Yesu; ni mbaya
kuliko hata mtu ambaye hajaokoka.
Hii inaonyesha ya kuwa unaweza ukaingia kwenye ndoa
ukapoteza wokovu wako, ukakosa kwenda mbinguni, si kwa sababu umefanya dhambi
ya uasherati, lakini kwa sababu umeshindwa kutunza watu wa nyumbani mwako, na
kwa ajili hiyo unahesabika kuwa umeikana imani.
Ukiangali kwenye Tito.2:3-5 anasema, “Vivyo hivyo na wazee
wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu, wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye
kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema, ili wawatie wanawake vijana
akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi,
na kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe,
ili neno la Mungu lisitukanwe”.
Unaweza ukaona kabisa ya kwamba Timotheo, anazungumza habari za
vijana wa kiume waliooa na wanafamilia, au umeoa na hujapata mtoto. Unao watu
nyumbani mwako, inawezekana ni msichana umeolewa, huu mstari pia unakubana.
Ukienda kwenye kitabu cha Tito, Tito anaandika moja kwa moja habari za wanawake
wazee, ili wawasaidie wanawake vijana, maana yake wasichana ambao ndio
wameolewa tu. Anasema, “Wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao
na kuwapenda watoto wao”.
Usingetegemea msichana aambiwe awapende watoto wao, hutaona
mwanaume anaambiwa awapende watoto, bali anaambiwa awalee watoto. Mwanamke
anaambiwa awapende watoto, ni kitu ninashangaa kila siku; maana nisingetegemea
mama aliyepata uchungu wa kuzaa aambiwe ampende mtoto. Watu waliookoka wengi
hasa wanapoingia kwenye ndoa, wanaingia kienyeji - kienyeji tu, hawajali ya
kwamba kuna kuwajibika.
Huwa ninawaambia vijana siku zote, hata kama mlikuwa mmezoea kutokula
nyumbani mwako, (maana kijana akiwa bado hajaoa, anaweza akakaa wiki au wiki
mbili, jiko lake halijawahi kupika kitu); kijana akiwa bado hajaoa, hakimsumbui
ana hela au hana hela, ataishi. Chakula kikiisha anaenda kutembelea ndugu na
jamaa, kama hawataki kumpa chakula, atakaa hapo mpaka amekula na ndipo aondoke.
Akikosa kabisa atajitia moyo kwa Bwana kwamba amefunga, na kumbe ameshinda
njaa!
Wakati mwingine mambo yakimzidia, na hana sabuni ya kufulia
nguo anasema hajali, kwa hiyo anaendelea, hana shida, anabadilisha nguo sio kwa
sababu amefua, lakini anabadilisha ili angalao jasho liweze kupungua hasa mnuko
wake, kwa hiyo anaitundika mahali ipigwe upepo usiku; na baada ya siku mbili
anavaa hiyo hiyo tena!
Huwa ninawaambia vijana siku zote kama hauko tayari
kuwajibika, usioe. Kwa sababu kama umeoa, haijalishi ya kwamba unafunga au
hufungi, chakula lazima kiwemo nyumbani mwenu. h haleluya! Na ukishaoa tu,
maana yake umeitangazia dunia nzima ya kuwa umeamua kuwajibika, na unaweza
ukatunza mke. Mambo ya kwenda kuomba -omba msaada tena inakuwa ni kitu ambacho
si wakati wake sasa. Maana unaposema, mimi nimeamua kuoa, maana yake umekubali
kuwajibika –na hii ni pamoja na kumlisha na kumtunza mke wako.
Ndio maana ukienda kwenye makabila mengine wanakuambia, ‘kijana
unataka kuoa umejenga nyumba?’ Nimeona makabila mengine wanauliza,
‘kijana wewe utaoaje wakati hata nyumba huna?’ Ndio maana vijana wanazuiwa kuoa
wakiwa shule, kwa nini, kwa sababu katika ndoa watahitaji kuwajibika. Sio kwa
sababu wakiwa shule hawawezi kuoa, ila ni kwa sababu wanajua suala la kuoa sio
kitu cha mchezo, linahitaji mahali ambapo unahitaji kuwajibika. Ndani yako
lazima uwe umekubali kuubeba wajibu uliomo katika ndoa!
Na kama ni msichana unataka kuolewa ukubali kuwajibika basi la sivyo
usikubali kuolewa kama hujawa tayari kuwajibika. Tito anawaambia wazi kabisa,
ya kuwa wafanye kazi nyumbani mwao wenyewe. Lakini sasa unataka hata kama
umeolewa, uishi maisha kama msichana, na hiyo ni hatari sana. Ukiingia kule
ndani ya ndoa kuna mabadiliko. Wakati ule ulikuwa unaosha vyombo vichache maana
ni vya kwako peke yako, sasa na mume wako yuko, na marafiki zake wamekuja
–vyombo vya kuosha vitaongezeka, na kuwajibika kwako kunaongezeka.
Ilikuwa inakusumbua kupika, unapika mara moja kutwa, na siku
hizi wataalamu wametuletea kitu kinaitwa ‘hot pot’, kwa hiyo hii mambo ya
kupasha pasha moto chakula siku hizi wakati mwingine hayahitajiki. Mtu ameweka
chakula chake anakifunika vizuri, anakuja jioni anakuta bado cha moto. Lakini
ninakuambia labda umeingia umeolewa na mtu ambaye ni mtumishi, ana wageni
nyumbani kwake kama kituo cha polisi, kila baada ya dakika mbili amekuja na
wageni wengine.
Labda mume wako ni mkarimu sana, kila mgeni akija anakuambia,
“fulani chai vipi?” Huko jikoni ‘unauma vidole’ maana umeshaingia jikoni
kuanzia asubuhi; labda saa hiyo ni saa tano, na umeshaingia jikoni kupika mara
nyingi, maana wageni wanapishana kila wakati. Kila saa ‘chai, chai’, unatamani
uondoke ili usiendelee kupika, lakini umebanwa – ndio kuolewa kwenyewe huko.
Ukiamua kuolewa kuwajibika kwako jikoni kutoangezeka zaidi.
Huwezi ukaamua tu saa yoyote ukasema, mimi nataka kwenda
kutengeneza nywele, huo muda wa uhuru wa jinsi hiyo umekwisha, ukitaka kwenda
kutengeneza nywele lazima uage, huwezi ukaondoka tu saa yoyote unayotaka, kila
kitu kinabadilika. Kuna masuala ambayo utahitaji kuwajibika nayo pale nyumbani,
huwezi kukwepa! Na kuna mambo mengine hakuna mtu mwingine ambaye atafanya kwa
niaba yako; kama usipotaka kuyafanya wewe.
Ndio maana watu wanafika mahali, msichana anaolewa lakini wiki ya
kwanza tu anataka msichana wa kazi wakati, hana hata mtoto mdogo. Unataka
msichana wa kazi wa nini, huo ni uvuvi tu. Lazima uwe mwangalifu, wewe umeolewa
tu, unataka msichana wa kazi, wa nini? Unaweza ukajitetea na kusema ni
kukusaidia kazi - kazi zipi? Unaweza ukajitetea na kusema, aa! Unajua
ninachelewa sana kutoka kazini, angalao nikute mtu wa kupika. Mimi
ninakumbia unaanza vibaya. Kama ndiyo kwanza umeolewa tu, na unataka wakumpikia
chakula mume wako awe ni msichana wa kazi, basi unaanza vibaya.
Wakati huo ndio saa ya kumtayarishia mume wako mapishi ambayo
hajawahi kuona kwenye nyumba ya baba na mama yake! Akikaa mwenyewe huku
anakula awe anasema, ‘ahsante Yesu kwa kunipa msichana wa namna hii!’ Kwa
sababu hajawahi kuona chakula kizuri cha namna hiyo ulichompikia - hata
hoteli hajawahi kukipata!
Lakini unaanza tu maisha ya ndoa na kumbandikia mume wako
watu wa kumhudumia, mimi ninakuambia unaanza vibaya, huko unakoelekea na ndoa
yako sio kuzuri. Uamuzi wa kuoa au kuolewa usiucheezee, kaa chini, fikiri
kwanza na kuomba kabla hujaamua.
No comments:
Post a Comment