Sehemu ya Nane
Jambo la Nane
“Je! Uko tayari kuolewa na nani”
“Je! Uko tayari kuolewa na nani”
Wengine hawafikirii namna hiyo, ukiwauliza uko tayari kuolewa na
nani, anasema na mtu aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu kwa
jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa alivyo kitabia. Maana
watu wengi sana wanasema wameokoka lakini hawajaokoka, wengine wanasema ‘bwana
asifiwe’ lakini ni bwana mwingine sio Bwana Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa
kufikiri, unataka kuolewa na nani.
Labda hujawahi kufikiria kitu cha namna hiyo, nataka nikufikirishe
vitu vya kawaida kabisa. Wengine wanasema mimi nataka kuolewa na mtumishi,
hesabu gharama kwanza! Wengine wanaona tunavyoshirikiana na mke wangu katika
huduma wanamtazama wanasema, wanataka kuolewa na mtumishi; kaamuulize mke
wangu, tulipokutana hata wito haukuweko, na tulikutana wote hatujaokoka.
Tulikuja kuokoka baada ya kuoana!
Mungu ametuteremshia utumishi tuko kwenye ndoa tayari, kwa hiyo
usitamani ndoa ya kwetu, tamani ya kwako ambayo Mungu amekupangia. Mke wangu
hakunipendea utumishi, sikuwa na tone la utumishi, wala hata ya kufanania ya
kwamba nitaokoka, na yeye alikuwa hajaokoka pia wakati huo. Lakini kwa
saa na kwa makusudi na kwa utaratibu wa Mungu, tumekuwa jinsi tulivyo.
Akatuteremshia utumishi wakati tumekwishaokoka na tumekwishaoana!
Usijaribu kufananisha ndoa yako na ndoa ya mtu mwingine,
hujui iliko toka, tamani ya kwako. Sasa unasema wewe unataka mtumishi, lakini
watumishi wako wengi sana, kwa hiyo unataka mtumishi wa namna gani? Lazima
ufikiri juu ya hili pia. Unasema mimi ninataka mhubiri, hata nabii ni mhubiri,
mwinjilisti ni muhubiri, mwalimu anaweza akahubiri. Kitabia hawafanani,
haleluya! Nataka nikufikirishe ikusaidie, maana nataka nikujengee msingi mzuri
wa maisha ambao ukikanyaga vizuri shetani alie tu, maana hatawezi kukuvuruga.
Maana watu wengi wanapata shida sana wanapotaka kuoa au kuolewa,
utakuta wanasema, mimi ninataka kuoa au kuolewa na mtumishi, hayo ni
maombi ya mtu ambaye hajaenda shule ya Roho Mtakatitu, bado yuko chekechea,
unajua lazima uwe ‘very specific’. Mungu anataka useme naye kile kitu
unachokisikia ndani yako. Anajua kabisa kitu ambacho ni kizuri kwa ajili yako;
lakini Mungu hataki kukulazimishia tu, anataka ushirikiane naye, ili akikupa
kitu ukipokee kwa furaha.
Kwa hiyo kama unataka mtumishi, ni muhimu useme unataka mtumishi
wa aina gani. Kwa mfano ukisema nataka mwinjilisti, hesabu gharama, lazima uwe
na neema ya kukaa na mwinjilisti. Si unajua mwinjilisti hakai nyumbani,
anazunguka, akikosa watu wa kuwachapa injili huko nje, anakuja kuchapa injili
nyumbani hata kama mmeokoka wote! Na ujue hawezi kumaliza ibada ya jioni mpaka
awepo mtu wa kutubu, hajatubu ataendelea kufanya maombi. Kama hauko
tayari kuchukuliana na mtu wa namna hiyo usiamue kuoa au kuolewa naye.
Lazima useme; au kama unataka kuolewa na nabii jipange, kwa sababu
hajui kuongea na watu, muda wake mwingi yuko kimya, manabii mara nyingi
wanafungwa midomo sio wasemaji ni mtu mkimya. Mara nyingi amejifungia kuomba
peke yake na Mungu. Hata saa nyingine unatamani uombe pamoja naye,
lakini Mungu anataka yeye peke yake. Wewe nenda kwenye biblia utaona
maisha yake yalivyo kila kitu kinachomzunguka, kila kitu anachovaa, kila kitu
anachokutana nacho, Mungu anaweza akakigeuza ujumbe.
Kwa hiyo usije ukashangaa kesho akakutazama na akaishia
kupata mahubiri toka kwako, halafu mkirudi nyumbani mnaanza kugombana, na
unamuuliza sasa wewe ulikuwa unanihubirije? Kwani wewe hukujua ya kwamba
ni nabii na anaweza kupata ujumbe unaosema: “kama vile mke wako alivyovaa,
ndivyo na kanisa langu lilivyo asema, Bwana”!
Wewe usifanye mchezo! Sasa nyingine mnaishiwa chakula na
anaona jinsi mnavyohangaika, basi utakuta amekwishapata ujumbe kama huu, “kama
vile mke wako alivyokuwa anahangaika kutafuta chakula kwa ajili ya watoto,
ndivyo na mimi ninavyotafuta chakula kwa ajili ya watoto wangu, asema Bwana”!
Saa nyingine unavaa nguo zinapasuliwa, mpaka viungo vya ndani
vinaonekana, ujumbe unatoka saa hiyo mara moja, anasema, “Kama vile mke wako
alivyovaa nguo iliyopasuliwa na watu wanaona ndani, ndivyo na kanisa langu
lilivyo vazi lake limepasuliwa na shetani anaona ndani”!
Lazima uwe tayari kuwa ujumbe, kama unataka kuolewa na
nabii. Uwe tayari kuwa ujumbe, hujawa tayari usiombe uolewe na nabii! Unataka
kuolewa na mchungaji uwe na moyo mkubwa wa kupokea wageni. Mwingine anasema
mimi ninataka kuolewa na mtumishi lakini ndani yake anawaza mtu anayezunguka na
kuhubiri, kumbe Mungu ameweka ndani yake mtumishi, lakini ni mfanya biashara.
Mfanya biashara mwingine anapakwa mafuta kufanya biashara, ndio
sehemu yake kumtumikia Mungu, mwingine ni fundi cherehani, mwingine ni dereva,
wanapakwa mafuta sehemu zao hizo za utumishi, usije ukafikiri hao wanaoafanya
kazi nyingine sio watumishi wa Mungu. Mungu anawapaka mafuta kwa ajili ya hizo
kazi, ili walitumikie kusudi lake.
Kwa hiyo unapokwenda katika maombi unasema tu mimi ninaomba
mtumishi, Mungu atakuletea mtumishi yoyote, wako wengi, wengine wanafagia
barabara, ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha kule kwenye vyoo vya
kulipia ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha nyumba za watu, nao ni
watumishi wa Mungu,oh haleluya!
Mungu akikuletea mtumishi yeyote unaishia kusema, mimi
sikuomba huyu niliomba mtumishi. Mungu atakuambia huyu ni mtumishi wangu,
usimnenee kitu cha namna hiyo.
Kama msichana ni mfupi usitamani kijana mrefu, au kijana ni mrefu
unatamani msichana mfupi. Kwa kweli, sio kwamba Mungu hawezi kukupa, lakini
wewe fikiri tu mwenyewe, haleluya! Maana mwingine anakuwa mfupi kiasi ambacho
anafanana kama vile ni mtoto kwako, wenzako wanakuuliza tangu lini umepata
mtoto na akakua na akawa mkubwa namna hii, unasema “ninyi msiseme hivyo,
ni mume wangu huyu”.
Ni uamuzi wako. Sasa, si lazima mfanane urefu, lakini
msipishane sana; kwa kweli ni kwa faida yenu wenyewe, haleluya!
Kama msichana hupendi mwanaume mwenye ndevu, omba vizuri. Maana
unaweza ukapata mtumishi wa Mungu, lakini ana ndevu na wewe huzitaki. Ikifika
siku umeingia tu kwenye ndoa kitu cha kwanza unamtafutia wembe ili anyoe ndevu
zake – hii ni kumwonea! Ulimpenda akiwa na ndevu, kumbe wewe ulikuwa unamtegea
tu ili baada ya arusi tu umpe wembe! Wako wasichana wanaopenda wanaume wenye
ndevu, waachie hao!
Huyu Bwana Mungu wetu ni mzuri sana, unajua, saa nyingine huwa
ninawaza jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na nabaki ninashangaa sana. Maana
kuna wanaume wengine hata ndevu hawana, hata wakilazimishia kunyoa kidevu
kitupu haziji. Sasa mtu mwingine anajisikia vibaya, akifikiri ya kuwa mtu
anaonekana ya kwamba yeye ni mwanaume kwa sababu tu ana ndevu, si kweli. Kuna wanaume
wengine wametengenezwa namna hiyo ‘special’ kwa ajili ya wasichana wasiotaka
wanaume wenye ndevu, haleluya!
Maana mwingine anaweza akaachia ndevu zikafunika mpaka
karibu na kwenye pua. Sasa kama ni mtu mweusi sana ‘ni hatari
sana’, giza likiingia tu ndani ya nyumba wewe unamwambia ‘cheka’, akicheka yale
meno yake yanaweza yakamulika kidogo, na utajua yuko wapi! Hivi vitu
ukishaingia kwenye ndoa ni vitu vikubwa sana, kuliko watu wanapoviangalia
kabla hawajaoana.
Wewe unakuta kijana anaoa msichana ana rangi nyeusi nzuri tu,
akifika ndani unamletea madawa ajikoboe, wewe ulikuwa unamwoa wa nini? Hiyo
sasa ni sawa na kumwambia Mungu kwa kweli nimechukua tu huyu, lakini sio
niliyekuwa namtaka!
Niliyekuwa namtaka ni mweupe, sasa maandamu umenipa huyu wacha
nimkoboe mpaka afike rangi ninayotaka, - haviendi namna hiyo bwana! Mungu
alipokuwa anamuumba huyo msichana namna hiyo aliona, alimtazama alivyo na weusi
wake huo akaona kila kitu chema, akajipa sifa, akajipa maksi asilimia mia moja,
amefanya kitu chema!
Sasa akitaka kupaka rangi hiyo ‘nyumba yake’ na
kuinakshi ni kitu kingine. Unajua kuna nyumba nyingine hazipendezi mpaka
uzipake rangi fulani, haleluya! Mwili ni nyumba, kuna wengine hawawezi
kupendeza mpaka wamepaka rangi fulani kwenye miili yao. Sasa utapata mtihani
mgumu, nimeona, kijana anampenda msichana, lakini msichana anaweka rangi kwenye
midomo yake, kucha zake anaweka rangi, anachora na kalamu hapa kwenye nyusi
kidogo, ukimtazama vizuri usoni utagundua ya kwamba ameweka kitu kingine juu ya
uso wake.
Umempenda akiwa namna hiyo. Wakati ulipokuwa unamfuatilia
hukumuuliza hayo maswali, leo ameingia ndani umemuoa, unamwambia sitaki hizo
rangi! Hiyo ni kumwonea, maana ulimkuta akiwa hivyo, kama ulikuwa humtaki
akiwa amejinakshi na rangi hizo, hukutakiwa kumfuatilia, wako wengine ambao
watakuwa radhi na huyo anayejipaka rangi!
Kuna kijana alioa msichana, wamefika ndani wakaanza kugombana naye
habari za nywele, mpaka akamrudisha kwao, - nywele tu! Huyu dada kaenda
katengeneza nywele staili fulani, yule kijana haitaki. Lakini alimkuta yule
msichana anatengeneza nywele kwa staili hiyo, sasa kwa nini hivi vitu
hawakutaka kuzungumza kabla ya kuamua kuoana?
Mimi ninataka nikusaidie upunguze ugomvi ndani ya ndoa
utakayokuwa nayo; maana vitu ambavyo Mungu atawaletea vya kufanya pamoja kwenye
ndoa ni vikubwa kuliko mnavyofikiri, kiasi ambacho hamhitaji kutumia muda wenu
kushindania vitu vidogo vidogo ambavyo mlikuwa muwe mmekwisha kuvijadili kabla
ya kuoana. Mna mambo muhimu sana ya kufanya, kiasi ambacho kuanza kushindana na
kubishana juu ya vitu ambavyo mlitakiwa muwe mumeshavizungumza kabla ya
kuoana; huko ni kutokuelewa utaratibu wa Mungu ulivyo juu ya kumpata mwenzi wa
maisha.
K
No comments:
Post a Comment