Sehemu ya Tisa
Jambo la Tisa
Uko tayari kuoa au kuolewa lini, maana yake ni
muda gani ambao ungetaka kuoa au kuolewa?
Uko tayari kuoa au kuolewa lini, maana yake ni
muda gani ambao ungetaka kuoa au kuolewa?
Utasikia mwingine anasema, siku Mungu atakapo nipa mume au mke,
hii ni hatari sana! Biblia inasema kwenye kile kitabu cha Mhubiri.3:1 “Kwa
kila jambo kuna majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.
Kila kitu kilichoko chini ya mbingu kimeratibiwa, kwa lugha
nyingine, ni kwamba kila mwanadamu ana kalenda yake, iko kalenda yako ya
kuzaliwa, na ipo kalenda ya matukio na mipango mbalimbali. Mungu anaijua.
Mungu anatangaza mwisho tangu mwanzo, anajua mwisho wa maisha yako wakati wewe
unapozaliwa.
Katika mwanzo wa maisha yako, Mungu anakuwa amekwishajua
mwisho wako; utakavyokuwa; na kama amekwishajua mwisho wako, maana yake
ameshatembea kwenye maisha yako yote toka mwanzo mpaka alipofika mwisho, na
alipokamilisha maisha yako akarudi mwanzo ndipo akakuongoza kuzaliwa.
Mungu anapokuacha uzaliwe duniani, hakika ujue kabisa ya kwamba
amekwisha tembea na wewe katika maisha yako, amesharatibu mambo yako na yako
hatua kwa hatua; kwa mfano, kitu gani utafanya, wapi utasoma, utasoma nini,
utaolewa na nani au utaoa nani na itakuwa, lini, maisha yako yatakuwaje,
utamtumikiaje, mpaka mwisho wako. Akiishafika mwisho wa maisha yako
anarudi mwanzo, akishafika mwanzo anatangaza mwisho tangu mwanzo; kwa hiyo
kuanzia hapo unapozaliwa ujue maisha yako yote yamesharatibiwa!
Ni vizuri ufahamu hii mistari itakusaidia, maana inakujengea
msingi mzuri wa maisha hapa. Isaya.46:9-10 inasema, “Kumbukeni mambo ya
zamani za kale maana mimi ni Mungu wala hapana mwingine, mimi ni Mungu wala
hapana aliye kama mimi. Nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za
kale mambo yasiyotendeka bado, nikisema, shauri langu litasimama, nami
nitatenda mapenzi yangu yote”.
Kwa lugha nyingine anatuambia ya kwamba, ‘wewe unaona kila kitu ni
kipya, unapoishi kila siku ni mpya, kila dakika inayokuja ni mpya, Mungu
anasema hiyo safari unayopita, mimi nilikwishaipita tayari, nikafika mwisho wa
maisha yako ndipo nikakuruhusu uzaliwe. Ulipokuwa unazaliwa nikatangaza mwisho
wako tangu wakati unazaliwa.
Sasa mimi ninataka nikuambie kama Mungu anajua, na shauri
lake anasema litasimama katika maisha yako, ili mapenzi yake ayatende katika
maisha yako, unahitaji kuwa mwangalifu. Kwa sababu kuna mpango na saa ya Mungu
ya kuoa au kuolewa, - ipo!
Mungu anapokuletea mawazo ya kuoa au kuolewa, ni kwa ajili
yakuimarisha maisha yako na wito wako na kazi na makusudi, ambayo ameyaweka
hapa duniani. Atakuletea mtu atakaye imarisha wito wako, atakuletea mtu atakaye
saidiana na wewe, uwe ni mwanamke au uwe ni mwanaume.
Mungu anapo kukutanisha na mtu wa kuoana naye ni kwa ajili ya
kuimarisha nguvu zenu ili mtimize kusudi la Mungu. Kwa hiyo lazima anajua kuna
saa huyu mvulana anahitaji mke, au huyu msichana anahitaji mume! Lakini watu
wengi sana hawalifuatilii hili. Wakati sisi tunaoana na mke wangu tulikuwa bado
vijana, tulioana hatujafikisha hata miaka thelathini, ninakumbuka nilikuwa na
miaka 28. Tulijaliwa kuwapata watoto tungali bado vijana sana. Lakini tuna
watoto ambao ni wakubwa kwa sasa. Tumefika kipindi ambacho tunaweza
tukafuatilia masuala ya utumishi kwa namna ambayo haiwaumizi watoto wetu sana!
Maana watoto wakiwa wadogo wote, mimi ninakuambia kumtumikia Mungu
ni kunakuwa kugumu sana, usije ukafikiri ni kurahisi. Maana unahitaji kuwa
karibu nao; wanahitaji kusoma shule, wanahitaji kufanya vitu mbalimbali,
wanahitaji kuwa na baba karibu, wanahitaji kuwa na mama karibu. Saa nyingine
mnataka kusafiri nao; unaweza ukasafiri nao lakini usije ukafikiri ni kitu
kirahisi.
Tulisafiri na Joshua
(mtoto wetu wa nne) akiwa na wiki sita. Sijawahi kuona watu wakisafiri na
watoto wao wakiwa wadogo namna hiyo, Joshua alikwenda kwenye huduma akiwa na
wiki sita tu. Hatukuwa na namna ambavyo tungeweza kumwacha. Sasa unaweza
ukaelewa akiwa na wiki sita; maana yake mama yake ana muda wa wiki sita tu
tangu ajifungue na tulisafiri kwa gari, sio kwa ndege, bali kwa gari!
Tulisafiri masaa karibu kumi na
mbili, tumebeba kila kitu, tumebeba mpaka unga wa kutengenezea uji, na beseni
la kuogea, na maji. Huwezi kumwogeshea mtoto mchanga wa wiki sita maji yoyote
tu, kwa hiyo tulibeba maji ya kumwogeshea. Huwezi kwenda ‘spidi’ unayotaka,
ikifika saa yake ya kula lazima usimame! Ukifika kwenye hoteli huwezi kumlaza
jinsi unavyotaka, lazima uingie kwanza uombe, uangalie yale mashuka
yaliyoko halafu uombe, uangalie kile kitanda halafu uombe, uangalie kila kitu
kule ndani halafu uombe!
Wewe ni mtumishi wa Mungu, ukienda na mtoto kienyeji
kienyeji tu, ibilisi anaweza akamvamia na ukapata shida, na huduma yako yote
uliyoiendea ikaharibika. Unaweza ukatamani saa nyingine usinge- safiri naye.
Lakini mnaposafiri pamoja, kumbuka ina gharama yake.
Lakini mambo haya unahitaji kufiri mapema, ili uweke kwenye
agenda yako ya maombi ujue kabisa mpango wa Mungu ya kuwa unatakiwa kuoa au
kuolewa lini. Ninajua kwa wengi kinakuwa kigumu hicho, maana wengine wametamani
kuolewa jana, hawajapata wanaume, wengine wangetaka kuoa leo, lakini bado
hawajapata msichana wa kuoa.
Wengine wanatamani kuolewa si kwa sababu mpango wa Mungu umefika
wa kuolewa; ila ni kwa sababu wanaona muda wao wa kuolewa umefika, wengine
wanaona umri umesogea. Mpango wa Mungu juu ya maisha yako, haubabaishwi na
jinsi wewe unavyohesabu miaka,jirani zako wanavyohesabu miaka, ndugu zako
wanavyohesabu miaka, au rafiki zako wanavyohesabu miaka.
Mungu anajua alichopanga kwa ajili yako, ana kalenda yako
kabisa, na kila alichokichagua Mungu ndicho sahihi.
No comments:
Post a Comment