Sehemu ya Saba
Jambo la Saba
Je! Uko tayari kuoa au kuolewa?
Je! Uko tayari kuoa au kuolewa?
Ni swali muhimu, uko tayari, maana yake umefika mahali hali yako
ya ndani na nje, inakuruhusu kuoa au kuolewa? Uko tayari kuoa au kuolewa? Umefika
mahali pa namna hiyo?. Wengine wanasema huyu ni mtoto, lakini unajua pamoja na
kwamba ni mtoto, ni vizuri kujua kama uko tayari kiumri. Lakini
ninapozungumzia hapa juu ya utayari wa kuoa au kuolewa, sizungumzii tu habari
za miaka, bali ninazungumzia habari za hali yako ya ndani.
Nimeona kuna mtu mwingine ana miaka arobaini, lakini kwa
kweli hayuko tayari kukaa na mwanamke, ndani yake, mawazo yake na kufikiri
kwake, hayuko tayari kukaa na mwanamke, hawajibiki hata yeye mwenyewe juu yake
mwenyewe. Wengine hata wana miaka hamsini, lakini ana hali kama hii. Nimeona
akinadada hata wana miaka arobaini na tano, hayuko tayari kuolewa, maana
akiolewa ni shida tu.
Nilienda mahali fulani, nikakuta dada ana umri mkubwa tu,
lakini wakati wa maombi hakusema kama anataka tuombe ili aolewe. Nikaona ngoja
nimuulize labda anaona aibu kusema hitaji hili kwa sababu umri umesogea,
nikamwambia “hutaki tuombe uolewe”? Akasema, “hapana, sitaki kuolewa” (Na
alikuwa ana umri wa miaka kama arobaini na zaidi). Nikamuuliza, “kwa nini”.
Akasema, “kwa sababu sitaki kuomba ruhusa kwa mwanaume ninapotaka kutumika”.
Nikamuuliza unafanya kazi, akasema, “ndio”.
Nikamwambia, “unapokwenda kumtumikia Mungu huwa unafanyaje, -
unaomba ruhusa au unatoroka huko kazini?” Akasema, “ninaomba ruhusa”.
Nikwamwambia, “kwa nini unaona ni rahisi kuomba ruhusa kwa mwajiri wako na
unaona taabu kuomba ruhusa kwa mume wako?” Alishindwa kujibu hilo swali.
Nikamwambia tatizo lako ni kubwa kuliko unavyo fikiri.
Unaweza ukaona kabisa ya kwamba, huyu mtu hayuko tayari kuolewa,
wala msijaribu kumlazimisha aoelewe – pamoja na kwamba umri wake ni
mkubwa. Usijaribu kumsukuma kwenye maamuzi ya kuolewa maana hayuko tayari
kuolewa, akiingia kwenye ndoa atakwenda kuleta shida tu!
Ndio maana ninakuuliza swali, je uko tayari kuoa au kuolewa?
Lina vipengele vingi vya kulitazama, na linabadilisha vitu vingi sana.
Mwingine unakuta ni msichana, wazazi wake ndio wanamtegemea karibu
katika kila kitu. Mimi ninakuambia kabla hujafikiria kuoa au kuolewa, fikiria
hilo swali. Kwa sababu ukiishaolewa tu biblia inakuambia wasahau watu wa
nyumbani mwa wazazi wako (Zaburi 45:10). Sasa haimaanishi usiwasaidie,
ila maana yake ni kwamba huwezi ukawasaidia tena ‘moja kwa moja’ kama
ulivyokuwa unawasaidia zamani. Ni vitu lazima ujadiliane na mume wako juu ya
kuwasaidia wazazi wenu wa pande zote mbili – maana mna mipango yenu sasa.
Na inawezekana labda umeoa au umeolewa kwa kijana ambaye hana
mzigo na wazazi wake kabisa, kila mtu anaishi kivyake vyake kama simba
porini, suala la kusaidia wazazi hana ndani ya moyo wake. Wewe umekuwa na
huo mzigo, wazazi wako wamekulea, umefika mahali umeanza kazi, sasa na wewe
unawatunza hatua kwa hatua, siku unaolewa yule baba anasema basi usiwatunze
tena, - fikiri hilo.
Litakuwa linakuumiza kila siku jinsi wazazi wako wanavyopata
shida. Utafika mahali utakuwa unachukua vitu kisiri siri unapeleka kwa wazazi,
na hiyo ina shida yake pia. Kwa hiyo kabla hujakubali kusema mimi nataka
kuolewa, fikiri kwanza na kuomba, maana ndoa inakwenda kukubadilishia mambo yako
mengi.
No comments:
Post a Comment