Sehemu ya Tatu
Jambo la Tatu
Ukiamua kuoa au kuolewa, wakati mwingine
imani yako inaweza ikabadilika.
Ukiamua kuoa au kuolewa, wakati mwingine
imani yako inaweza ikabadilika.
Wasomaji wa biblia wanamfahamu mtu mmoja aliyeitwa mfalme Sulemani
(unafahamu ni kwa nini aliandika kitabu cha Mhubiri, maana alipoandika kitabu
cha Mhubiri akasema, mambo yote chini ya jua ni ubatili mtupu). Biblia
inatuambia wazi kabisa ya kuwa Mungu alimpa hekima ya ajabu, na wasichana
wakatoka sehemu mbali mbali duniani kwenda kufuatilia ile hekima, walipoikuta
hawakutaka kuondoka na wakabaki pale kwake.
Kosa alilofanya Sulemani ni kwamba wale wasichana walikuwa
wanakuja na miungu yao, na alikuwa anawakaribisha wale wasichana na miungu yao,
anawapa na mahali pa kujengea vibanda vya miungu yao. Biblia inatuambia wazi
kabisa, ilifika mahali wale wakina mama wakamgeuza moyo wake usiendelee
kumpenda Bwana.
Kitabu cha 1 Wafalme 11:4 kinasema hivi: “Maana ikawa,
Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine,
wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba
yake.”
Nimeona vijana wengi sana ambao wanakuwa moto sana kwenye wokovu
kabla hawajaolewa au kuoa, wewe ngoja waingie kwenye ndoa na wafuatilie
baada ya muda, utakuta wengine wamepoa mpaka wameganda kama barafu!
Ukiwauliza ni nini kimewafanya wapoe kiroho kwa kiwango hicho - wanaweza
wakashindwa kusema. Maana kuna watu wengine wanafikiri ni kuolewa tu na mtu
yoyote kwa sababu tu anasema Bwana asifiwe, ibilisi Pia huwa anaweka na watu wa
kwake huko ndani ya makundi ya watu waliookoka.
Na ukikaa na vijana utapata baadhi yao wanaosema, ukitaka kupata
vijana waaminifu siku hizi nenda katikati ya waliokoka, kwa hiyo wanajifanya
wameokoka. Akikufuatilia juu ya kuoana na ukimwambia mbona wewe hujaokoka, na
ukamtaka kwanza aokoke ndipo mzungumze, utakuta baada ya siku chache kupita
anajifanya ameokoka, lakini ni yakubabaisha tu ili akupate. Nimekutana na
watu wa namna hiyo, msichana anaolewa akishafika ndani, ndio kijana anamwambia,
na Yesu wako na wokovu wako nauvua hapa hapa, mimi nilikuwa nakutafuta wewe,
nimekupata basi!
Nimeona! Sisemi kitu cha hadithi, ninasema kitu ambacho
nimeona kwa macho. Ikiwa umefika katika hali hii basi, ni mpaka kifo
kiwatenganishe, na alikwishawaambia wenzake kwamba Mungu amenifunulia; kwa hiyo
hana ujasiri wa kurudi na kusema kweli nilikuwa nimekosea, yalikuwa ni mafuniko
sio mafunuo! Akitaka kwenda kwenye maombi anaambiwa hakuna; akitaka kwenda
kuhudumu anaambiwa hakuna; anataka kwenda ‘fellowship’, anaambiwa hakuna; kaa
hapo ndani. Kwa hiyo inabaki kazi moja tu ya kuombea chakula na chai na kwenda
kulala!
Na ni kwa sababu huyu mtu hakufikiri sawasawa, hakukaa
akaona jinsi ambavyo hili jambo linaweza likambadilishia imani yake kabisa.
Wewe nenda kwenye maandiko, utaona ya kuwa ndoa inaweza ikakubadilisha. Ndio
maana kuna watu wengine wanaolewa, na wengine wanaoa na wanabadilisha dini, hii
sio kitu cha mchezo, ni maamuzi magumu sana kuyafanya.
Unapobadilisha imani yako unabadilisha msingi wako kabisa wa
maisha yako; kwa hiyo ni lazima uamue jambo ya kuoa au kuolewa kwa uangalifu
sana.
Lakini pia inaweza ikawa ni mkristo kwa mkristo wanataka kuoana,
lakini fahamu kuoa au kuolewa kunaweza kukakubadilisha dhehebu lako la
kikristo, ndio maana lazima mkubaliane juu ya jambo hili kabla ya kuingia
kwenye ndoa. Nilikuta vijana wamekubaliana kuoana, kijana mmoja mlutheri,
kijana mwingine mpentekoste. Mambo yakawa magumu sana kwao, walipofika masuala
ya kujadiliana, juu ya imani zao. Ilikuwa ngumu sana, mpaka wachungaji
wao wakaingilia kati.
Walipokuja kuniona, nikawauliza mko tayari kabisa na mnataka
kuoana? Wakasema, ndio. Wakati huo walipokuja kwangu walikuwa tayari
wameshaenda nyumbani kwao, wameshazungumza na wazazi wao, na kote huko na
wakati wote huo hawakufikiria hilo jambo. Sasa imefika mahali mchungaji wa
kanisa hilo la pentekoste hakubali msichana wake aolewe kwa kijana wa
kilutheri. Nikamuuliza maswali yule msichana akashindwa kujibu.
Unajua wapentekoste hawabatizi watoto, walutheri wanabatiza
watoto. Mnapooana matokeo yake ni kwamba watoto watazaliwa. Ni lazima hicho
kitu ufikiri kabla hajasema ndio kuolewa, au ndio kuoa. Sio umekwisha olewa
ndipo unasema watoto wangu hawawezi kwenda huko, - ulikuwa wapi toka mapema ili
uliseme hili tatizo? Maana unaweza ukafikiri ni masuala marahisi, sio masuala
marahisi.
Maana wengine wanalichukulia jambo hili kirahisi, wakati jambo
lenyewe sio rahisi. Masuala ya kwenda kusali kanisa tofauti tofauti huku
mmeoana sio mambo rahisi. Nimeona watu wakisema hakuna tatizo maana
tutaoana, lakini kila mtu wetu atakuwa anakwenda kanisani kivyake; sawa, ninyi
mnaweza mkaenda kivyenu, na watoto je? Labda kama hamna mpango wa kuzaa!
Maana niliona kwenye TV, mtu mmoja, - dada mmoja huko ulaya
amefuga mbwa akasema, tuliamua huku ndani tusizae watoto na badala yake
tumefuga mbwa badala ya mtoto, wamempa na jina, wamempa na chumba wamempa na
kitanda, anasahani yake, na bajeti yake, ana daktari, wameamua wasizae na
badala yake, wamefuga mbwa! Labda kama unataka kuelekea njia hiyo! Lakini kama
unaingia kwenye ndoa na unajua utakwenda kupata mtoto, suala la mahali
mnapokwenda kusali ni muhimu sana kulijadili na kuliamua kabla ya kuingia
kwenye ndoa.
Usiende kupeleka vita kwenye ndoa yako ambayo haitakiwi kuwepo!
Unajua kuna vita vingine tunavianzisha bila sababu, hata Yesu alijua, wakati
saa yake ya kupigwa mawe ilipokuwa haijafika, alikuwa anawakwepa wale watu
waliokuwa wamepanga kumpiga mawe. Sasa kama Yesu alikuwa anakwepa majaribu
mengine kwa nini wewe unajitumbukiza? Saa ikifika ya jaribu kuja kwako
utalishinda tu, kwa sababu umetengenezwa na Mungu uwe na uhakika wa ushindi,
kwa sababu ukiwa ndani ya Kristo unashinda na zaidi ya kushinda.
Imeandikwa hivi katika kitabu cha Warumi 8:37; “Lakini
katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye
aliyetupenda”. Lakini majaribu ya kujitafutia, yanaweza yakayumbisha
imani yako.
Maana watu wengi sana huwa hawajiulizi hili swali mapema lakini
nimeona likiwapa shida. Wengine hata imefika saa ya kufunga ndoa, ndio
kwanza wanaanza kujiuliza, ‘ndoa sasa tunakwenda kufungia wapi’, hilo sio
swali la kujiuliza saa hiyo, utakuwa umechelewa! Wewe ulikuwa unajua kabisa
mwenzako anasali mahali fulani, na wewe unasali mahali pengine, imefika saa
mnataka kufunga ndoa mnaanza kujiuliza, tukafunge ndoa kwenye kanisa la nani,
ikiishafika hapo mnaanza kushindana na kuvutana; na haifai mambo kuwa hivyo.
No comments:
Post a Comment