Sehemu ya Sita
Jambo la Sita
Uamuzi wa kuoa au kuolewa unaweza wakati mwingine
kukuletea marafiki au maadui.
Uamuzi wa kuoa au kuolewa unaweza wakati mwingine
kukuletea marafiki au maadui.
Sasa nakufikirisha hivi vitu vikusaidie, inawezekana kabisa
hujafikia umri wa kuoa au kuolewa, lakini ninakuambia weka maombi yako ya
akiba, (sijui kwa upande wako, lakini mara nyingine huwa nawaombea watoto wangu
maombi ya akiba, kwa ajili ya ndoa zao kama Yesu atakuwa hajarudi, kwa sababu
najua maana yake ni nini).
Ni vizuri upate maombi ya namna hii mara kwa mara - ujiombee
mwenyewe, ukipata watu wa kukuombea shukuru Mungu, lakini hata kama hujapata
watu wa kukuombea, ninakuambia kazana kujiwekea maombi ya akiba. Hiyo ni njia
panda. Mahali pa kuoa au kuolewa ni njia panda. Ukichagua njia ambayo haiko
sawasawa, maisha yako yatakuwa magumu sana.
Sasa ukiangalia kwenye kitabu cha Hesabu.12:1-2 inatuonesha wazi
kabisa ya kwamba, harusi ya Musa ilileta ugomvi katikati yake na ndugu zake,
hasa dada yake na Haruni. Kilichowasumbua ni kwamba alikwenda kuoa mwanamke
Mkushi; au amekwenda kuoa mahali ambako hawakutarajia, kwa hiyo wakakasirika.
Halafu naamini Musa aliwaambia Mungu amesema naye juu ya kuoa mke huyu, wale
watu wakasema, ‘Mungu anasema na Musa tu peke yake, haiwezekani’ - ugomvi
ukaingia.
Unajua ugomvi uliingia kiasi ambacho Mungu akasikia yale maneno na
hayakumfurahisha, akawaita kwenye hema. Ikabidi ajieleze wazi uhusiano wake na
Musa.
Kitabu cha Hesabu 12:6-8 kinasema; “Kisha akawaambia,
Sikilizeni basi maneno basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA,
nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa
mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; kwake
nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA
yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?”
Alivyomaliza kusema namna hiyo dada yake Musa akapata ukoma!
Ugomvi umetokea wapi? Musa alipooa! Kwa kuwa ameoa msichana
ambaye dada yake hakumtaka. Mungu alimtaka, lakini dada yake hakumtaka. Dada
mtu akaanza kumsema kaka yake, Mungu akampa adhabu! Dada mtu alipopewa adhabu
ile na kaka mtu akapata shida, Israeli nzima ikapata shida, hawakusafiri
walisimama wote, hawakuendelea na safari. Ugomvi ulitokea wapi? Ulitokea mtu
mmoja alipooa!
Nimeona ndoa zingine kijana anaoa lakini uhusiano wake na
baba yake na mama yake unakatika wakati huo huo. Vijana wengine wanakuwa hawako
waangalifu hapo, na ndio maana mambo yakiwa magumu, na wazazi wanawabishia juu
ya kuoa au kuolewa kwao hawataki kwenda kuzungumza na wazazi wao;
wanapiga ‘short cut’, wazazi wao wanakuja kuambiwa tu saa na tarehe ya harusi!
Biblia inasema, “waheshimu baba na mama yako, hii ni amri ya
kwanza yenye ahadi ili upewe siku nyingi katika nchi upewayo na Mungu wako”
(Waefeso 6:1). Na kwa sababu hiyo vijana wengi sana wakiishakorofishana wazazi
wao hawaendelei katika ndoa muda mrefu wakiwa na amani.
Sasa sisemi kwamba wamkubali tu huyo msichana au huyo kijana, ni
zaidi ya hapo unajua. Suala ninalozungumzia hapa ni la wao kukupa kibali, na
wakafurahi. Unaweza ukasema, hawaelewi kitu au hawajaokoka, kwa hiyo hawahitaji
kuelezwa kitu. Hapana!
Ndio maana unahitaji kuomba. Kwa sababu unajua suala la kutaka
kuleta msichana au kijana ndani, sio la kwako peke yako, linawahusu wazazi wako
na ndugu zako kwa sababu unawaingiza kwenye familia nyingine. Hata kama unataka
kuoa au unataka kuolewa, ni mambo ya kifamilia maana ni koo mbili
zinakutanishwa na kuunganishwa.
Wakati mwingine unaunganisha kabila mbili au unaunganisha kabila
tatu, (wengine hawaelewi kitu ninachosema, kwa mfano; “Mimi ni mnyakyusa,
mke wangu ni msukuma, watoto wangu ni kabila gani”? Wanakabila mbili, ni
mchanganyiko wa wanyakyusa na wasukuma, maana ningetaka kujipendelea ningesema
ni wanyakyusa.
Lakini ndani wanaunyakyusa na wanausukuma halafu waolewe na mtu wa
kabila lingine ambalo sio mnyakyusa wala sio msukuma, ni makabila mangapi
yanaungana hapo, matatu! Sasa fikiria na anayeoa kwangu na yeye awe
ametoka kwenye mchanganyiko wa namna hiyo.
Unaunganisha hapo makabila matatu, manne, matano, sasa wewe
unataka wazazi wako wasiifuatilie ndoa hiyo kwa karibu. Kwa nini? Ukipata shida
utarudi kwa wazazi wako, sasa kwa nini wakati wa maamuzi wasikusaidie!
Na mimi ninakuambia iko njia ya kutokea, ikiwa utapata
tatizo la namna hii; wewe kukaa kwenye maombi kwa namna ambavyo, kama ni Mungu
kweli aliyekupa huyo msichana au aliyekupa huyo kijana, basi ataweka kibali
hicho hicho ndani ya wazazi wako, ili na wao wamkubali.
Saa nyingine unaweza ukapata marafiki wengine wazuri, lakini
wakati mwingine marafiki wengine wanakuwa ni wabaya. Maana ukishaolewa marafiki
wa mume wako ni marafiki zako, ukishaoa marafiki wa msichana ni marafiki zako.
Vijana siku hizi wanaotaka kuoa au kuolewa wakitaka kujua ukoje, hawakuangalii
wewe wanaangalia marafiki zako. Marafiki ulionao ndio wanaoonyesha picha
uliyonayo ndani yako.
Rafiki wa kweli hafuati pesa ulizonazo, anafuata tabia uliyo nayo,
wale marafiki wanaokufuata kwa sababu unacho kitu cha kuwapa hao sio marafiki,
wanakufuata kwa sababu unachokitu, siku ukiishiwa huwaoni. Lakini wale marafiki
unakuwa nao wakati wa shida na wakati wa raha, ni marafiki ambao malengo yenu
na tabia zenu, kufikiri kwenu kusema kwenu zinafanana. Hao ndio marafiki ambao
wanakuwa marafiki zako wa kweli; siku ukiwa na shida ni marafiki zako, unahela
ni marafiki zako, umefilisika ni marafiki zako, hao ndio marafiki zako!
Sasa kama mtu anataka kukuangalia ulivyo, anaangalia
marafiki zako. Sasa, akiangalia marafiki zako, hata kama unasema, ‘Bwana
asifiwe’, hata kama unapiga pambio mpaka jasho la damu linatoka, lakini
wanaangalia marafiki zako ulionao, na wakati mwingine ni wabaya kuliko wale wa
kule duniani, wanajua na huyu msichana au huyu mvulana kuna mahali ‘ana short’.
Kwa wengine inakuwa vigumu kuliona kwa namna hii, lakini ni lazima
ufahamu ukiwa kama kijana, lazima uwe mwangalifu juu ya marafiki ulionao.
Vijana wengine wanabaki kushangaa kwa nini wasichana wanahangaika wanasema
hatuoni vijana wa kuwaoa, wakati vijana wapo, lakini nani ataolewa
na vijana ambao wameokoka lakini hawana msimamo? Nani anataka kijana wa namna
hiyo ambaye anashinda vijiweni sawasawa na hao vijana wengine wa duniani?
Mwanaume akitaka kuoa lazima ajifunze
kuwajibika. Hawezi akawa na marafiki ambao hawawajibiki kimaisha – na akataka
aone na aendelee na urafiki nao. Akiwa karibu na hao marafiki, itakuwa ni
vigumu kuwa na ndoa yenye amani. Angalia tu marafiki alionao, unashangaa kwamba
anaendelea kusema bado ameokoka. Unashangaa wale marafiki alionao, hawafananii,
hawawezi hata kumtia moyo kuomba, hawawezi kumtia moyo kusoma neno, vitu
wanavyozungumza ni vitu vya ajabu.
Unajua, hata wakati mmoja hawana maneno
ya kutiana moyo ya kuwa na maendeleo binafsi, lakini ndio anaoshinda nao toka
asubuhi mpaka jioni, halafu anataka kuoa msichana ambaye ameokoka, anayeshinda
kwa Mungu , anayekaa kwenye maombi, anayetaka kuona cha Mungu kinasimama katika
maisha yake, ndiye anataka kwenda kwake ili amuoe;- hii siyo sawa! Ndoa
yao itakuwa na matatizo tu kwa muda mrefu.
Maana usije ukapata shida ukiingia kwenye ndoa na kijana wa
namna hiyo. Wewe uliona kabisa marafiki zake walivyo, unaolewa na ndipo
unaposema, ‘mimi sitaki hao marafiki zako’! Imeanza wapi? Atakuambia vizuri
kabisa “ulinikuta nao”, kwa nini hukusema mapema kabla hatujaoana ya kuwa
huwataki?
Msichana anaolewa na ndipo kijana anamwambia hao marafiki zako
nisiwaone hapa, lakini alikuwa anawakuta chumbani kwako wakati alipokuwa
anakuja kukutembelea na hakusema kitu, na wakati mambo yakiwa magumu katikati
yenu alikuwa anawatumia wao kukubembeleza ukubali kuolewa naye, sasa
umekwishaolewa hawataki. Anaanza kuwasema ya kuwa tabia zao sio nzuri.
Hili jambo si zuri; alitakiwa aseme mapema juu ya kutoridhika kwake na rafiki
zake.
Unapotaka kuoa au kuolewa, usifikirie tu picha ya yule mtu
wakumuoa au kuolewa naye, ni vizuri kuangalia na aina ya marafiki zake wa
karibu – je unaweza kuchukuliana nao?.
No comments:
Post a Comment