Sehemu Kumi na Moja
Jambo la Kumi na Moja
Uko tayari kuishi katika hiyo ndoa kwa muda gani?
Uko tayari kuishi katika hiyo ndoa kwa muda gani?
Sasa ninakupa siri hapa ikusaidie, Kama umekaribia – karibia kuoa au kuolewa,
na hujawahi kujiuliza maswali ya namna hii, basi Mungu anakuweka mahali pazuri
kwa kukupa nafasi ya kusoma kitabu hiki. Labda nikuambie kitu cha namna hii
kitakusaidia, kabla sijakupa mistari mingine kwenye biblia, ni hivi: Hakuna
sababu ya kuolewa na kijana ambaye atakufa baada mwezi mmoja. Au hakuna sababu
ya kuoa msichana atakayekufa muda si mrefu baada ya arusi yenu.
Kwa nini uolewe leo uwe mjane baada ya miezi miwili? Na
ukiishaolewa umekwisha badilisha kabisa hali yako na ya mume wako;
akiisha kufa wewe sio msichana tena, utaitwa mjane, hata kama umri wako ni
mdogo. Tulienda mahali ulani tukasema tunaomba wajane tuwaombee, tulishangaa kuona
ya kuwa robo tatu yao walikuwa ni wasichana. Ungeambiwa wameolewa ungekataa,
lakini wamefiwa bado wana umri mdogo.
Sasa mimi ninataka nikuulize swali, kwa nini unataka uolewe,
halafu mume wako afe baada ya miezi miwili au unataka uoe mke wako afe baada ya
mwezi mmoja, au baada ya mwaka? Hakuna kitu kinachosumbua kama hiki. Ngoja
nikueleze hili tena ya kuwa ndoa ya pili sio ndoa ya kwanza. Ndoa ya kwanza ina
utofauti wake, na ndoa ya pili ina utofauti wake.
Ikiwa
unataka kuishi muda mrefu na mwenzi wako wa ndoa unahitaji;
1. Kuwa
mwangalifu kutii ile mistari ilioko kwenye biblia inayozungumzia juu ya muda wa
mtu kuishi. Kwa mfano: Waefeso 6:1-3 inasema; “Enyi watoto, watiini wazazi
wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri
hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, upate heri, ukae siku nyingi katika
dunia”.
Kwa hiyo angalia uhusiano wako na wazazi
wako kama bado wako hai. Lakini pia chunguza uhusiano wa huyo anayetaka kukuoa
au anayetaka umuoe, na wazazi wake, kama bado wako hai.
2. Omba Mungu akupe maisha marefu
na huyo mwenzako hata kabla hamjaamua kuoana. Ili kama kuna mmoja wenu hataishi
muda mrefu – basi Mungu awaarifu na kuwaongoza cha kufanya.
Mwingine anataka aingie kwenye ndoa kwa kubahatisha au kwa
majaribio. Maana yake ndani ya nafsi yake anajiweka tayari kuachana na mwenzi
wake kama anaona mambo ya ndoa yake hayaendi alivyotarajia. Mtu wa namna hii
hataweza kuwa mvumilivu na mwepesi wa kutafuta suluhisho kukitokea tatizo
katika ndoa yake.
Uamuzi wa kuoa au kuolewa unamtaka mtu aingie katika ndoa asilimia
mia moja. Ikiwa hautakuwa tayari kuingia kwenye ndoa kwa asilimia mia moja –
tafadhali usiamue kuoa au kuolewa. Utampotezea tu mwenzako – maana hakuna ndoa
isio na matatizo. Lakini pia hakuna tatizo ambalo Mungu hawezi kulitatua.
Lakini, je, uko tayari kushirikiana na Mungu katika ndoa kwa kiwango cha
asilimia ngapi?.
No comments:
Post a Comment