Sehemu ya Kumi
Jambo la Kumi
Uko tayari kuzaa, kutunza na kulea watoto wangapi?
Uko tayari kuzaa, kutunza na kulea watoto wangapi?
Niliuliza vijana fulani ambao ndio wametoka tu kuoana, wanafurahia
maisha yao, ghafla nikawauliza swali ambalo hawakutegemea, nikawauliza,
“mna mpango wa nakuzaa watoto wangapi? Walinitazama wakasema, “Mungu anajua”.
Nikawambia; “siyo hivyo! Mungu anajua lakini ninyi je?” “Wakasema hatujui”,
nikawaambia hayo ndio makosa ya wengi waliomo katika ndoa.
Sasa ninakueleza hivi kwa sababu ni vitu ambavyo Mungu alisema na
sisi mapema. Hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kuokoka ambaye
sikujua ya kwamba atazaliwa, na hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kukuokoka
ambaye sijajua wito wake. Na Mungu aliponyamaza na hakutuonyesha mtoto
mwingine, hatukuona sababu ya sisi kutafuta mtoto mwingine. Wengine
wanafikiri Mungu hana mipango ya uzazi (kasome biblia yako vizuri) – Mungu ana
utaratibu wa uzazi kwa kila ndoa anayoisimika.
Ni kitu ambacho unahitaji kuomba, ili Mungu akujulishe. Nimeona
watu wakishindana ndani ya ndoa, baba anataka watoto wengi, mama hataki.
Nimekuta ndoa nyingine mama anataka watoto wengi wamzunguke kama timu ya mpira
lakini baba hataki. Na ugomvi mkali unatokea juu ya hili.
Mwingine anamzalisha mke wake kila mwaka (unaelewa maana ya kila
mwaka?) si unaelewa mimba inakaa miezi tisa tumboni, kwa hiyo anaweza akazaa
kila mwaka! Sasa umewahi kufikiri kila mwaka unazaa, kwa hiyo ikiwa uko kwenye
ndoa miaka kumi basi una watoto kumi. Au mtu yuko kwenye ndoa miaka mitano,
tayari ana watoto wanne na bado anaendelea kuzaa – hii ni sawa?
Nilikwenda mahali fulani kwa ajili ya huduma dada mmoja alikuwa
anafurahia muujiza wake wa tumbo, jinsi ambavyo Mungu amemponya, akasema, “sasa
nitakuwa tayari kuzaa mtoto mwingine”. Nikamuuliza, “una watoto wangapi sasa?”
Akasema, “wanne”. Nikamwambia, “Na bado unahitaji mtoto mwingine”. Akasema,
“ndio, ninataka mtoto mwingine”! Unajua kwa nini ninakueleza vitu vya namna
hii, - kwa sababu kila mtoto ana wajibu wake, ana mzigo wa kwake na anatunzwa
kivyake!
Kadiri unavyozaa watoto wengi, ndivyo unavyozidi kuwa na wajibu
mkubwa zaidi wa kulea. Watoto hawafanani, huwezi ukawalea kijumla. Watoto
hawalelewi kwa namna hiyo. Kila mtoto ameitwa kivyake, ana mpango wake, ana
njia yake, ana tabia yake na ana namna yake ya kutunzwa,– hawafanani!
Mtoto anayezaliwa lazima umlee kwa uangalifu. Hujamfikisha mahali
katika kumlea, tayari ameshakuja mwingine, unafikiri mchezo!
Hao watoto wawili hujawafikisha mahali katika kuwalea tayari
ameshakuja mwingine, ni kitu kigumu hujawahi kuona! Huyu wa kwanza hapati tena
ule umuhimu wake na nafasi yake, kwa sababu sasa anakimbiliwa huyu aliye
mdogo; akija mwingine anakimbiliwa aliye mdogo zaidi, hao waliotangulia
wanajikuta wanakua kivyao.
Watu wengi wanabaki kushangaa kwa nini watoto wengi
waliozaliwa kwa kufuatana saa nyingine kwa karibu wanagombana. Ni kwa sababu
huyu mkubwa anaona ameingiliwa na huyu mdogo, na huyu mdogo anaona kwamba huyu
mkubwa ameshakuwa mkubwa, kwa hiyo mimi niliye mdogo ndiye mwenye haki zaidi.
Ni ugomvi unaoweza ukaendelea mpaka wamekuwa watu wazima.
Mimi nimesoma masuala ya uchumi, sijasomea masuala ya
kuhubiri. Si kwa sababu sikupenda kusomea kuhubiri, lakini hakuwa mpango wa
Mungu wa kunilea namna hiyo katika wito. Kuna wengine Mungu anawapanga na kulea
wito wao kwenye vyuo vya biblia; na ni mpango wa Mungu tu mzuri. Lakini Mungu
alikuwa na mpango mwingine na mimi. Mimi katika chuo nilikwenda kusoma
masuala ya uchumi.
Sasa, siku moja nchi hii ilitembelewa na wageni, wa kutoka
Washington D.C, wa shirika la fedha ulimwenguni. Wale watu wakatuuliza maswali,
hebu tuambieni mabadiliko ya uchumi yanayoendelea hapa nchini ninyi mnayaonaje.
Mama mmoja akanyoosha mkono, akasema, “Tunaelewa umuhimu wa
mabadiliko mengine yanapotokea katika uchumi wa nchi, kwa sababu ya mazingira
tunayoyaona hasa tunapoona vitu vingine havifanyi kazi. Kwa hiyo kuna umuhimu
wa kubadilisha sera zingine ili mambo yaende sawasawa.
Lakini tatizo tulilonalo, ni kwamba maandalizi ya kutuandaa sisi
kama watanzania ya kwamba kuna mabadiliko yanakuja, hayo maandalizi
hayajafanyika ya kutosha”. Wakasema, “mama tupe mfano”. Akasema “kwa mfano,
tunatakiwa kuchangia masuala ya afya, tunatakiwa kuchangia masuala ya elimu,
kama tungejua kwa mfano, miaka mitano au sita kabla, kwamba miaka sita ijayo au
miaka kumi ijayo, ya kuwa pamoja na kwamba sasa elimu ni bure, afya ni bure,
iko siku mtahitaji kutoa pesa zenu mfukoni ili kulipia gharama hizi – tungekuwa
waangalifu tunazaa watoto wangapi.”
Nikagundua mara moja kwamba huyu mtu wazo lake lilikuwa ni
zuri kabisa.Kwa sababu kwa watanzania wengi inapofika mtoto anazaliwa walijua
anayewajibika kumpeleka huyo mtoto shule ni serikali, anayewajibika kumlipia
gharama za hospitali ni serikali! Wewe
utazaaje ili serikali ikutunzie mtoto? Lazima na wewe uwe na bajeti yako!
Unajua biblia haisemi serikali leeni
watoto, inaasema enyi wakina baba leeni watoto. Soma Waefeso 6:4. Sasa
pale serikali itakapokusaidia wacha ikusaidie, lakini usikae unajiambia ya kuwa
mimi nimezaa watoto kumi na tatu, lazima waende shule bure, lazima waende
kwenye hospitali bure. Nani anayegharamia hizo huduma, unafikiri ni za bure?
Hakuna! Wewe unaona huduma hizo ni bure, lakini yuko mtu ametoa pesa za
kugharamia hizo huduma toka mahali fulani.
Nakumbuka wakati fulani nlikuwa
Zimbabwe, baba mmoja aliyekuwa na cheo kikubwa tu kwenye makanisa ya kule
Zimbabwe, tulikuwa tunazungumza naye siku moja juu ya masuala ya kusomesha
watoto. Alisema wakati mmoja alikwenda Ujerumani kwenda kutafuta watu wa
kuwasomesha watoto wake.
Yule mzungu ambaye alikuwa anazungumza naye,
akaamuuliza, “ndugu una watoto wangapi, akasema sita”. Akasema, “unajua mimi
nina watoto wangapi.” Akasema, “sijui”. Akasema watoto wawili”. Akasema,
“unajua ni kwa nini hatutaki kuzaa watoto wengi, usije ukafikiri tunachukia
watoto, hasha ila ni kwa sababu ya gharama, za kuwatunza zilivyo kubwa”.
Tunataka angalao kila mtoto atunzwe
vizuri na aende shule nzuri, wakiishakuwa wengi inakuwa si rahisi kuwagharamia
wote ipasavyo, na inabidi ugawe ulichonacho kidogo kidogo. Wanaishia wote
shule ya msingi, kwa sababu huna hela ya kuwapeleka sekondari. Akasema, “sasa
ninyi waafrika mambo yenu hayako sawa, wewe unaona mimi nimezaa kidogo nimejinyima
kwa ajili ya watoto wangu wasome vizuri, sasa unataka fedha ya kwangu
nikusomeshee watoto wa kwako ambao wewe umezaa bila kufikiria jambo la gharama
ya kuwatunza wakiishazaliwa?”
Aliambiwa kitu cha kweli usoni na
mzungu! Unaweza ukafikiri alikuwa anamtukana, lakini alikuwa anamweleza kitu
cha ukweli; watu wengi sana hawafikiri hiki kitu. Wale wazee wa zamani walikuwa
wakizaa kwa mahesabu huku nyuma. Akizaa watoto wa kike wengi ana hesabu ng’ombe
atakazopata watakapoolewa, usije ukafikiri ana hesabu gharama, bali ana hesabu
ng’ombe atakazopata! Watoto wa kike kwake ni mradi. Akizaa watoto wa kiume
anajua amepata nguvu kazi ya kulima mashamba, walikuwa wana mahesabu yao.
Lakini sasa hivi lazima ukae ufikiri kwa
namna nyingine,sikuambii ya kwamba kuwa na watoto wengi ni kitu kibaya, ni
uamuzi wako! Kama unataka kwenda na mstari unaohimiza mkaongezeke mkaijaze nchi
(Mwanzo 1:28) hakuna shida! Unaweza ukaendelea na wewe ukawa kwenye kuijaza
nchi, lakini usikazane kuijaza nchi halafu unataka wengine wakusaidie kulea
watoto hao - hiyo sasa sio sawa!
Mimi sijui kwa upande wako, na sijui
kwa upande wa wazazi wako, lakini ninakueleza ili baadaye uwe mzazi mzuri, ni
vitu unahitaji kufikiri mapema. Niliwaambia watoto wangu siku moja, nikawaambia
sikiliza, tumejiwekea maamuzi ndani ya hii nyumba mimi na mama yenu, ya
kwamba ni wajibu wetu kuwasomesha mpaka chuo kikuu ili angalau kila mmoja awe
na shahada ya kwanza, huo ni wajibu wetu.
Baada ya shahada ya kwanza ukitaka
kuendelea Mungu akubariki. Mungu akitupa nafasi ya kukusaidia kuendelea zaidi
ya shahada ya kwanza tutakusaidia. Lakini tumemwomba Mungu atusaidie, kila mtu
lazima afike chuo kikuu. Unajua kama usipoweka malengo ya namna hii, hata
matumizi yako na bajeti yako haviwezi kukaa sawa. Ndio maana ninakuambia lazima
umwombe Mungu akusaidie, usije ukafikiri kusomesha watoto ni kitu rahisi.
Ninyi mnajua ambao mko shule, wengine
wameshindwa kuendelea na shule kwa sababu wazazi wameshindwa kutoa karo za
shule, na sio kwa sababu wanafunzi hawataki kuendelea na shule, lakini ni kwa
sababu hakuna fedha za kuwasomesha.
Nilimuuliza msichana mmoja katika mkoa mmoja wakati nilipokuwa
huko kwa huduma, nikamuuliza “umemaliza darasa la ngapi”. Akasema, “kidato cha
sita”. Nikamwambia, “sasa kwa nini hutaki kuendelea na shule?” Akanitazama
usoni, halafu akasema, “sithubutu hata kumwambia baba anisomeshe zaidi
maana ninawaangalia wadogo zangu huku nyuma walivyo na ninaangalia na
hali ya baba yangu aliyonayo kifedha, amenisaidia nimefika kidato cha sita,
sasa nikifikiria wadogo zangu – ambao bado wako shule za msingi, naona wacha na
wao basi wasogee sogee angalau wafike sekondari na wao kama mimi. Kwa hiyo mimi
nimenyamaza kimya”.
Huyu msichana amemaliza kidato cha sita anataka kuendelea na
masomo, lakini hawezi kuendelea kusoma kwa sababu anaangalia hali ya wazazi
wake ilivyo, anajua kabisa angalau na wadogo zake na wao wasome, lakini sio
kwamba anataka kuishia kidato cha sita.
No comments:
Post a Comment